Monday 21 January 2019

MAMBO MUHIMU YANAVYOPELEKEA MAVUNO MAZURI YA SAMAKI

  MAMBO 7 MUHIMU YANAYOPELEKEA  MAVUNO MAZURI YA SAMAKI




   Kama mfugaji wa samaki unapaswa kuzingatia mambo haya muhimu ili uweze kupata faida na mavuno mazuri ya samaki:-
  
Uchaguzi sahihi wa mbegu za samaki, kutapelekea kuvuna samaki wakiwa na uzito sahihi ndani ya muda sahihi uliokusudiwa.

➽Kupandikiza samaki wako kwa idadi maalumu ndani ya bwawa lako, hii itapelekea samaki kukua vizuri kwa kuwa watapata nafasi na hewa ya kutosha ndani ya bwawa.

➽Kulisha chakula kilicho na virutubisho vizuri na vilivyo changanywa kwa uwiano kulingana na rika la samaki husika na aina ya samaki mwenyewe mfano kama ni samaki sato tengeneza chakula kutokana na jamii ya samaki hao usiwape samaki wengine,fuata kanuni bora za ukaushaji wa chakula na uhifadhi ili kisipoteze ubora wake.

➽Lisha samaki wako kwa wakati maalumu na ulioshauriwa na wataalamu ambapo kwa wastani wa mifumo mingi ya ufugaji ni asubuhi kuanzia saa 2 - 4 na jioni kuanzia saa 10-12 jioni, usilishe samaki wako asubuhi sana na jioni sana wakati jua limezama.

➽Lisha samaki wako chakula cha kutosha washibe
kiwango cha chakula wanachopaswa kupewa hutegemea na uzito wa samaki husika mfano samaki akiwa mdogo wastani wa gramu 20 atakula kidogo kulinganisha na samaki mwenye uzito wa gramu 200, ni muhimu sana kufahamu idadi ya samaki wako na uzito wao ili uwape chakula kutokana na vigezo muhimu vya uzito na idadi.

➽Badilisha maji kwa wakati pale tu unahisi yamechafuka, dalili za awali maji kuchafuka ni kuwa na rangi ya ukijani uliokolea na dalili nyingine maji kutoa harufu , hivyo unapaswa kufuata kanuni na taratibu za ubadilishaji wa maji.

➽Hakikisha ulinzi unakuwepo muda wote kwenye mradi ikiwemo kuweka wavu juu ya bwawa ili kuzuia ndege ,kenge na fisi maji (otters) au kwa lugha iliyozoeleka VICHECHE, kufanya hivi kutapelekea kuvuna samaki wako kwa idadi  ile ile ulio pandikiza awali ndani ya bwawa lako.

   Haya ndo mambo muhimu unayopaswa kujua ili uweze kufanikiwa katika ufugaji wa samaki ukizingatia haya na kanuni na taratibu zote nyingine za ufugaji kutapelekea mavuno mazuri ya samaki na kupata faida. 

@Article by Musa Ngametwa

  

No comments:

Post a Comment