Thursday 28 February 2019

UJENZI WA BWAWA LA KUFUGIA SAMAKI

UJENZI BORA WA BWAWA LA SAMAKI

   Ni jambo muhimu sana kuchagua eneo zuri kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la samaki ili kufanikisha na kurahisisha kwa urahisi kazi ya kufuga samaki. Si kila eneo la ardhi hufaa kwa kazi ya kufuga samaki. 

 Bwawa linaweza kuchimbwa kwa mkono au kwa mashine, njia zote mbili ni sahihi isipokuwa kama bwawa ni kubwa au unakusudia kufuga kibiashara ni vema ukatumia mashine kwa sababu mashine inafanya kazi kwa haraka na hivyo kumaliza mapema, pia ufanisi wake unakuwa ni mkubwa ukilinganisha na na ufanisi wa bwawa linalochimbwa kwa mkono.

                                             Ujenzi wa Bwawa la Samaki

             SIFA ZA ENEO LA KUJENGA BWAWA LA KUFUGIA SAMAKI


Kwa Bwawa la kusakafiwa kwa udongo wa mfinyanzi hizi ni baadhi ya sifa muhimu sana za kuzingatia katika chaguzi sahihi la eneo:-


➧Liwe karibu na chanzo cha maji salama.

➧Liwe kwenye eneo lenye udongo wa mfinyanzi kwa sababu hauruhusu maji kunywea kirahisi.

➧Liwe katika eneo lenye mteremko kidogo (si lazima sana) ili uwezeshe maji kutiririka kutoka na kuingia bwawani.


Kwa Bwawa la kusakafiwa kwa simenti hizi ni baadhi ya sifa pia muhimu sana za kuzingatia katika ujenzi katika eneo husika:-


➧Liwe na karibu na chanzo cha maji salama.

➧Liwe katika eneo lenye udongo wa mfinyanzi (si lazima sana), uwiano kati ya mchanganyo wa simenti,mchanga na maji wakati wa kutengeneza bwawa la samaki lililo sakafiwa kwa simenti.
            
➧Ni muhimu sana kwa kiwango cha simenti,kokoto kuwa kikubwa zaidi ya kiwango cha                       mchanga na maji ili kuepukana na tatizo la bwawa kupoteza maji kwa mda mfupi.


       KANUNI NA TARATIBU ZA UTENGENEZAJI WA BWAWA LA KUFUGIA SAMAKI

 Ili uweze kufanikwa katika ujenzi bora wa bwawa la kufugia samaki unapaswa kufuata kanuni na taratibu zote katika ujenzi huo.

⥈BWAWA LA UDONGO

Kwa Bwawa la udongo unapaswa kufuata kanuni na taratibu hizi ili uweze kutengeneze bwawa zuri na lenye viwango:-

➧Chagua eneo zuri lenye sifa.

➧Pima udongo.

➧Pima maji.

➧Fanya usafi wa eneo la kujengea bwawa lako (ondoa visiki na vikwazo vinginevyo).

➧Fanya vipimo vya ukubwa wa bwawa lako kulingana na mahitaji yako na ukubwa wa eneo                 lako.
           
➧Zingatia unapofanya vipimo kumbuka kwa kila sqm 1ya bwawa lako utapandikiza samaki                    watatu.

                                     
 Pandikiza majani ya kutosha kwenye kuta.kingo na migongo ya bwawa lako ili kuimarisha bwawa lako lisiharibike kirahisi na mmonyoko wa udongo. Hakikisha unashindilia vizuri kuta,kitako na migongo ya bwawa lako (tumia vitu vizito vya kushindilia ili kuiamarisha zaidi).

 Zoezi hili litafanywa kwa muda wa wiki mbili mpaka tatu likiambatana na zoezi la kumwagilia maji kwa kiasi kidogo sana kwenye kuta ili kuziimarisha na pia kufanya nyasi zako ziote na kukua kwa haraka.


Zingatio: Kama udongo wako si imara kuhifadhi maji basi hakikisha unatandika plastiki maalum katikati ili kuepusha hasara ya upotevu wa maji mara kwa mara.


⥈BWAWA LA SIMENTI

Kwa Bwawa la simenti unapaswa kufuata kanuni na taratibu hizi ili uweze kutengeneze bwawa zuri na lenye viwango:-

➧Chagua eneo zuri lenye sifa.

➧Fanya usafi wa eneo la kujengea bwawa lako (ondoa visiki na vikwazo vinginevyo).

➧Fanya vipimo kama ni bwawa la usawa wa ardhi basi vipimo vyake ni sawa na lile la udongo,vitatofautiana kwenye matumizi ya simenti,kokoto na maji. Kama ni kisima kwaajili
ya vifaranga kitaanzia usawa wa ardhi kwenda juu kwa 1m.


Kumbuka:Katika aina zote hizi za mabwawa usisau kuweka mabomba maalumu makubwa na yenye unene wa kutosha na imara kwaajili ya kuruhusu maji kuingia na kutoka, pia na mfuniko wa nyavu au waya ili kuzuia samaki kutoka wakati wa kubadilisha maji ama wakati wa uvunaji.

Pia usisahau kuweka shimo dogo litakalo kurahisishia wakati wa uvunaji.


        UANDAAJI WA BWAWA LA SAMAKI KWA AJILI YA KUPANDIKIZA SAMAKI


➧Kausha bwawa lako lote.

➧Weka madini (kemikali) kwa ajili ya kuuwa vijidudu acha likae kwa muda wa wiki moja.

➧Jaza maji bwawa lako (robo tatu ya bwawa).

➧Weka mbolea ya kuku kidogo kwenye kiroba kilichotobolewa matundu madogomadogo na juu kifunge na kamba, kitumbukize kiroba hicho ndani ya bwawa kwenye ukingo mmoja na uache kiroba hicho kwa siku kadhaa huku ukipima kiwango cha urutubisho wa bwawa lako (search disc ama mkono).

➧Ukiona ukijani umeshajaa wakutosha (usizidi sana) toa kiroba nje.

➧Pandikiza samaki wako kwa kutumia vipimo vya uwiano maalum kwa kupandikiza samaki kulingan na ukubwa wa bwawa.


FAIDA NA HASARA ZA UCHAGUZI WA AINA YA BWAWA LA KUFUGIA SAMAKI


 Bwawa lililosakafiwa na Udongo wa     Mfinyanzi

Faida zake:

 Mkulima anapunguza gharama ya ulishaji (samaki hupata chakula cha asili ndani ya bwawa).

 ➧Gharama ndogo za ujenzi.

 ➧Uzalishaji mkubwa wa hewa safi.

 ➧Kiwango cha joto si kikubwa.


Hasara zake:

Uimara (sio imara zaidi ukilinganisha na bwawa la simenti).


  
                 Bwawa lililosakafiwa na Simenti

Faida zake:

Ni imara.

Hasara zake:

➧Samaki wanategemea zaidi chakula toka kwa mfugaji (uzalishaji wa chakula cha asili ni hafifu).

➧Gharama za kulitengeneza ni kubwa pia lina mahitaji mengi zaidi.

➧Pia kiwango cha joto wakati wa jua kali huzidi (hivyo  humpa mkulima gharama ya kununua               mashine ya kuzalishia hewe safi ndani ya maji).



  Uchimbaji wa bwawa la kufugia samaki inasisitizwa kuwa ni vizuri ukazingatia maelezo ya kitaalamu katika uchimbaji wa bwawa ili uweze kufanikiwa katika kazi hii ya ufugaji wa samaki na kupata mavuno mengi zaidi ya samaki ukiwa na bwawa imara.


No comments:

Post a Comment