Friday, 21 December 2018

UFUGAJI WA SAMAKI KWA KUTUMIA NJIA ZA KISASA ZINAZOZINGATIA UHIFAHDI MAZINGIRA, KATIKA ENEO DOGO NA GHARAMA NAFUU:



Ndugu mfuatiliaji wa fululizo za masomo ya AAS ufugaji wa samaki ni teknolojia inayokuwa kwa kasi sasa katika nchi yetu pia yaweza kuwa ni njia moja wapo itakayosaidia katika juhudi za kutunza mazingira,kukuza kipato na pia kuunga mkono juhudi za Raisi wetu wa awamu ya Tano Dr. John Joseph Pombe Magufuli za kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Leo tutajifunza aina za ufugaji wa samaki kwa njia za kisasa na za gharama nafuu pia zinazingatia uhifadhi wa mazingira (aina hii ya ufugaji ni rahisi hata kwa Mtanzania mwenye eneo dogo,anayeishi katikati ya mji anaweza kufuga bila shida yeyote):

UFUGAJI WA SAMAKI KWA KUTUMIA MABWAWA TURBAI YA PLASTIC/MABWAWA YANAYO HAMISHIKA:
 
Aina hii ya ujenzi wa mabwawa hutengenezwa kwa kutumia turbai maalumu za plastic pamoja na pomba za chuma zinazopindwa na kutengenezwa kuwa katika umbo la mraba ama mstatili,mabomba haya huwa na ukubwa tofauti ili yaweze kuvaana kirahisi na kutoa umbo la bwawa na kuchomolewa kirahis wakati wakuhama ili kumrahisishia mfugaji kutokufungwa kufanya kazi sehemu moja.Aina hii ya mabwawa ujenzi wake na ufungwaji wake wa mabomba unafanana sana na ufungwaji wa mahema.

MUONEKANO WA BWAWA LA KUHAMISHIKA:

 


FAIDA ZA UJENZI HUU WA MABWAWA:
 
    Yana gharama nafuu kwa upande wa ujenzi hivyo humsaidia mfugaji kutumia gharama ndogo katika ujenzi.Hapa mfugaji hatakuwa na gharama za kununua cement,nondo,kokoto,mchanga wala kutafuta mashine za kuchimba,anachotafuta ni bomba za chuma na turbai nzito ya plastic basi.

    Yanazingatia uhifadhi wa mazingira,hapa mfugaji hatachimba ardhi kwani yenyewe huanzia juu ya uso wa ardhi,pia kama ni mfugaji anayetumia kemikali katika ufugaji wake kwenye chakula ama kutibu samaki basi aina hii ya mabwawa inakinga kemikali zile kudhuru ardhi na viumbe wengine waishio arhini (Angalizo ili kutimiza hili pindi tu mfugaji anapoona plastic sheet imechakaa na anataka kubadii nyingine anapaswa kuzingatia sana utupaji wa mifuko hiyo sehemu sahihi na si kuiacha izagae ovyo,ni mbaya kwenye mazingira,ni vyema akaikusanya na kuiweka sehemu moja ili iunganike na takataka nyingine kwaajili ya matumizi mengine ama kufanyiwa recycling)

    Faida nyingine ya mabwawa haya huruhusu ufugaji kufanyika katika eneo dogo  kwa unadhifu Zaidi.Hii hufungua fursa ya ufugaji wa samaki kwa wakazi waishio katikati ya miji wenye maeneo madogo.


UDHAIFU WA UJENZI HUU WA MABWAWA:
  Mfugaji asipokua makini wakati wa uchaguzi wa turbai anaweza pata turbai zilizo chini ya kiwango na kuleta usumbufu wa kupasuka na kuvujisha maji mara kwamara.

   Pia plastic ina sifa ya kupata joto sana wakati wa jua kali hivyo kwa wafugaji waishio maeneo ya joto  akiwa amepandikiza samaki wengi kupitiliza ndani ya eneo dogo joto liliongezeka samaki wataathirika,ni muhimu kama ni mfugaji wa maeneo ya joto awe makini kufuatilia mabadiliko ya hali joto ya maji kwa kupima temperature mara kwa mara ili aweze kuzuia athari hizi.

USHAURI KWA WAFUGAJI WANAOISHI VIJIJINI,PEMBEZONI MWA HIFADHI ZA BAHARI NA HIFADHI ZA WANYAMA PORI NA MAZINGIRA KWA UJUMLA:
 
Kwa matokeo chanya ya ufugaji wako na pasipo kuleta uharibifu wa mazingira ni vizuri kutumia ufugaji huu katika hali ya ufugaji mseto (intergrated fish farming)  kwani utakupa faida kubwa kwakua ufugaji huu mseto unaleta mtegemeano mkubwa wa kiikolojia pia hautaaribu mazingira.
Mtegemeano wa kiikolojia unaotokea:
Unapofuga kuku ama bata pamoja na samaki kinyesi cha kuku ama bata utakitumia kutengenezea chakula cha asili kwenye bwawa(algae,phytoplankton,zoo plankton) lakini pia wakati wakubadili maji kwenye bwawa badala ya kumwaga maji ovyo,maji hayo kumbuka yana virutubisho vingi,mbolea nyingi ambayo ni nzuri sana kwenye ukuaji wa mimea hivyo unaelekezea bomba la outlet kwenye bustani yako yaweza kuwa ya mbogamboga,matunda,nafaka kama mahindi ama miti ya a mbao ambavyo vitakupa faida ya chakula pia na fedha,Zaidi ya hapo unapo vuna mazao yako kama mahinndi mabaki ya majani na magunzi hautatupa utawapatia mifugo yako kama nguruwe na wengineo hii itakusaidia kuepukana na migogoro ya kuachia mifugo ovyo kwenda ndani ya maeneo ya hifadhi lakini pia itakusaidia katika utunzaji mazingira kwani utajikuta hautaacha takataka ama mabaki yeyote ovyo kwenye mazingira,kila kitu kinakuwa na matumizi yake kwa mtegemeano huo wa kiikolojia ya viumbe uliyoitengeneza.   


Ahsante kwa kufuatilia masomo yetu,kwa msaada wowote usisite kuwasiliana nasi.






Thursday, 1 March 2018

UFUGAJI SAMAKI MSETO

MKOMBOZI KWA WAFUGAJI WENYE KIPATO KIDOGO!!


Hii ni moja kati ya aina za ufugaji wa samaki wa kutumia gharama nafuu na kuleta faida kubwa kwa wafugaji. 
Aina hii ya ufugaji samaki huenda sambamba na shughuli nyinginezo za kilimo, ufugaji kuku,bata ama nguruwe katika eneo moja ama katika maeneo yaliyokaribiana sana..



 Aina hii ya ufugaji ni ufugaji pekee ulio katika mfumo maalumu wa mlishano wa kutegemeana kati ya samaki unao wafuga,nguruwe,kuku,bata na kilimo utachofanya.Hivyo humpunguzia gharama nyingi sana mfugaji kwani hatakuwa na uhitaji wa kununua mbolea nje kwaajili ya kurutubisha bwawa wakati wa uaandaaji wa bwawa kabla ya kupandikiza vifaranga,mbolea itakayopatikana toka kwa kuku,nguruwe ama bata itatumika kurutubisha maji kwenye bwawa kwaajili ya uzalishaji wa mimea ya majini  (phytoplankton)ambayo ni muhimu sana katika ukuaji wa samaki,lakini vilevile mbolea nyingine itatumika moja kwa moja kwenye mazao kwenye shamba la miti,matunda na vilevile katika bustani ya mbogamboga.

Mbali na hapo katika aina hii ya ufugaji maji machafu yanayo tolewa wakati wa kubadilisha maji toka kwenye bwawa hapa huwa hayamwagwi ovyo,yanaongozwa na mabomba ya kutolea maji ama mifereji toka kwenye bwawa na kuelekezwa kwenye bustani ya mbogamboga na maeneo mengine yenye mazao kama miti ya matunda na mbao iliyozunguuka katika eneo la shamba lako (Maji haya yana mbolea na virutubisho vingi sana hivyo husababisha mimea kubadilika kwa haraka kuwa kijani Zaidi na  kukuwa kwa haraka).

 Vile vile matope,majani,wadudu na takataka nyinginezo zinazotoka ndani ya bwawa wakati wa kubadili maji hutumika kama chakula kwa nguruwe na kuku badala ya kutupwa.
Hivyo unaweza ukajionea aina hii ya ufugaji ilivyo nzuri katika swala la kubana matumizi kwa kuhakikisha kila rasilimali iliyopo inatumika vizuri kwa manufaa ya mfugaji na viumbe husika vinavyofugwa,kuhakikisha eneo lote la shamba lako na rasilimali zote zinatumika kwa manufaa pasipo kutumia gharama kubwa za uwendeshaji mradi.

Aina hii ya ufugaji ni mkombozi hasa kwa wafugaji wenye kipato ama mtaji mdogo,pia aina hii ya ufugaji ni rafiki na mazingira yetu kwa kiasi kikubwa haisababishi uharibifu wa mazingira ukilinga nisha na aina nyinginezo nyingi(sehemu kubwa inajiendesha yenyewe kwa kutumia vitu asili vilivyoko katika mazingira ya kawaida mashambani).

 Aina hiii ya ufugaji mseto pia humpa nafasi kubwa mfugaji ya kuweza kupata faida kubwa Zaidi na kupanua mradi wake kwani anakuwa anafanya shughuli Zaidi ya moja zinazo tegemeana kwa wakati moja na kumletea mavuno endelevu ya bidhaa tofauti kwa vipindi tofauti(mavuno tofauti yasiyokuwa ya msimu na kwa mazao tofauti). 

Mfano:
Mfugaji anapokuwa amefuga samaki aina ya sato ama kambale kwa wingi sambamba na ufugaji kuku wa kiasi,pamoja na kilimo cha mbogamboga kwa eneo dogo lililozunguuka mabwawa yake,eneo kubwa la shamba lililobaki akapanda miti ya matunda na mbao kama tiki(hakika baada ya miezi sita ataanza kuvuna samaki,mbogamboga na matunda na kama akiwa walizingatia upandikizaji wa vifaranga kwenye mabwawa kwa muda tofauti hii itampa uvunaji endelevu wa samaki kwenye ma bwawa yote kila baa da ya miezi sita),Kikubwa Zaidi ni kwamba wakati huwo miti ya mbao na matunda itakuwa ikiendelea kukuwa(miti kama tiki  kwa muda wa miaka kuanzia kumi unakuwa na uhakika wa hela ya kutosha),Miti hii itakusaidia kama mtaji mkubwa utakao kuza mradi wako wakati ujao ili uweze kufuga kisasa Zaidi na kuwa na teknolojia ya kisasa ya ufugaji samaki kwa faida kubwa(kwa mfumo huu unampa fursa mfugaji mwenye kipato kidogo kuwa na uhakika wa kutimiza malengo yake)


             Mpangilio mzuri wa ufugaji samaki mseto kwa mradi mkubwa:




Kwa mawasiliano/mualiko wa kuendesha semina n.k tupigie ama tuandikie kupitia:

+255(0)764175381, +255(0)713199655


Tuesday, 26 December 2017

VIUMBE WAHARIBIFU KWENYE UFUGAJI WA SAMAKI,MAGONJWA SHAMBULIZI NA HATUA SAHIHI ZA KUDHIBITI (KINGA NA TIBA)

VIUMBE WAHARIBIFU NA MAGONJWA YA SAMAKI NA JINSI YA KUEPUKANANAYO

     
       Viumbe wa haribifu kwenye bwawa la samaki si wengi  sana japo kuna malalamiko bado yanayojitokeza toka kwa wafugaji.

      Viumbe kama chura, Ndege, Kenge, Kicheche na wengineo wamekuwa wakiripotiwa kuingia marakawamara kwenye mabwawa na kula samaki.

           Zifuatazo ni mbinu rahisi za kufanya  ili kuepukana na tatizo hilo;

UDHIBITI WA VIUMBE WA ARDHINI KAMA CHURA  KENGE, NYOKA NA WENGINEO

  •    Unapotengeneza bwawa lako hakikisha unachimba mfereji wa kina kidogo kwenda chini kuzunguka bwawa lako lote , mfereji huo tandika karatasi ya nailoni ili kuzuia upotevu wa sumu ya ya maji kama unatumia sumu ya maji na kwa anayetumia ya unga kuna haja ya kutandika karatasi hiyo ili kuepusha uharibifu wa mazingira( kemikali zisizohitajika ardhini).  
  •    Umbali toka kwenye bwawa hadi kwenye mfereji angalau  uwe 1m kutoka kwenye bwawa ili kutoruhusu mdudu amakiumbe chochote cha ardhini kuvuka mpaka wako kisha jaza maji yenye sumu ama sumu ya unga.                    

           UDHIBITI WA VIUMBE WA ANGANI HASAHASA NDEGE

       Tengeneza  fremu ya mabanzi yenye ukubwa uliozidi bwawa lako kidogo litakaloweza kufunika eneo lote kuzunguka bwawa lako kisha tumia nyavu yenye matundu madogo kama zile zinazotumika kutengeneza madirisha ya nyumba lakini haikikisha matirio yake ni nailoni inayotumika kwenye uvuvi ili kuongezea uimara isioze mapema kisha wamba nyavu hiyo juu ya fremu yako na igongee kwenye kingo za fremu yako ya mabanzi kisha funika juu ya bwawa lako, hii itatumika kama ufuniko mda wote ili kuzuia viumbe wa angani waharibifu kama vile ndege kushindwa kuingia wala kuchukua samaki kwenye bwawa lako wakati wote.

MAGONJWA SHAMBULIZI KWA SAMAKI NA NJIA ZA KUEPUKANA NAYO 

           Moja kati ya mifugo isiyoshambuliwa sana na magonjwa ni samaki,lakini pia ni moja kati ya viumbe wanaoweza kuambukizana magonnjwa kwa urahisi endapo moja akiathirika na magonjwa na hatua za kumnusuru zisipochukuliwa mapema.


 Malalamiko mengi toka kwa wafugaji ni juu ya fungus,samaki hushambuliwa na fungus hasa kwa samaki wadogo kwa mfano kambale wakati wakuzalisha kwa njia ya kisasa kwa maana utalazimika kuweka mayai  na kuacha vifaranga kwa wiki chache kwenye eneo dogo ili kuwatengenezea mazingira bandia yanayoendana na mazingira asili ili wazaliane(mfano unaweza kufanyia kwenye aquarium yenye kichanja,taa ya joto kwaajili ya kuzaliana),kwa muda huwa mara baada tu ya mayai kuanza kuanguliwa huwa  wanaendelea kula kiini cha yai kwa siku chache za mwanzoni bila kutumia chakula kingine na baadaye atermia kabla ya kuwatoa na kuanza kuwapa chakula cha kawaida,kipindi hiki upo uwezekano mkubwa sana wa fungus kuzaliana kwa wingi na kushambulia samaki kutokana na uwepo wa viini(yolk) na maganda ya mayai ndani ya maji hivyo kupelekea maji kuwa machafu,eneo pia ni dogo,huleta ongezeko la joto,ukiunganisha na uchafu wa taka mwili za samaki hutengeneza mazingira mazuri kwa fungus na bacteria kuzaliana kwa wingi ndani ya maji na kushambulia samaki (mara nyingi huathiri idadi kubwa ya vifaranga wanaoanguliwa kisasa ndani ya aquarium na kuwasababishia vifo maana huambukizana kiurahisi kutakana na maji hutumika kama kisafirishi cha ugonjwa), hili huleta malalamiko mengi toka kwa wafugaji samaki wengi hudai kwanini wakifanya uzalishaji wa kitaalamu kwa kambale huzalisha samaki wengi sana lakini hawakui wote na wengi wanakufa katika hatua hii ya utoto?


   Jibu ni hilo na pia yatupasa kukumbuka kuwa kinga ya mwili dhidi ya magojwa kwa viumbe wadogo ni ndogo haiwezi kulingana na viumbe wakubwa,hivyo inahitajika umakini sana wakuwa karibu na samaki wako hasa wakiwa katika hatua hii ya utoto,zingatia sana usafi wa maji,joto,kiwango cha kemikali ndani(acid na base) na ulishaji,ukiwa makini na hivi hakika utafurahia ukuaji wa samaki wako wote.

     Kwa samaki wakubwa vivyohivyo huathiriwa na fungus japo ni kesi chache sana hutokea kwa samaki wakubwa ambazo kwa sehemu kubwa husababishwa na uzembe wa kuto kuzingatia usafi wa maji ndani ya bwawa.



       NJIA ZA KUFANYA ILI KUEPUSHA TATIZO HILI

           Hakikisha unabadilisha maji ndani ya wakati maalum,pima usafi wa maji mara kwa mara kwa kutumia search disc ukigundua yameanza kubadilika rangi sana na huioni vizuri ndani ya nusu mita jua maji ni machafu na badilisha.

          Lakini vile vile si uchafu wa maji kwa kuonekana kwa macho tu,pia unatakiwa uwe umejijengea tabia ya kupima hali ya kikemikali ya maji mara kwa mara(yaani kiwango cha acid,base,chumvi,joto)hivi huweza kubadili hali joto ya maji,kuongeza sumu kama ammonia(kutokana na uchafu kama kinyesi toka kwa samaki) na kutengeneza mazingira mazuri kwa vijidudu kama bacteria kuzaliana kwa kasi na magonjwa ya ngozi kama fungus na mengine kuongezeka na  kushambulia samaki wako.

      DALILI ZA MAGONJWA HAYO NI KAMA ZIFUATAZO

        ⧫Samaki kubadilika rangi ya ngozi

        ⧫Samaki kutoona vizuri na macho kuwa na ukungu

        ⧫Samaki kujawa na uteute uliopitiliza juu ya ngozi yake.

     ⧫Samaki kukatikakatika baadhi ya viungo vyake kama   mikia

        ⧫Samaki kubabukababuka ama kuchubuka ngozi

        ⧫Samaki kujitenga na kuwa katika hali dhoofu.
Hizi ni baadhi ya dalili kuu ziko nyingine nyingi.....    

   

           NINI KIFANYIKE UKIGUNDUA HALI KAMA HII

  ⧫Mtenge haraka samaki uliye muona na dalili hizo ili asiwaambukize  wenzake(mtoe na muweke kwenye bwawa ama chombo cha pekeyake.

  ⧫Badilisha maji kwenye bwawa hilo na lifanyie usafi wa uhakika bwawa lako,ikiwezekana tumia lime ama dawa nyinginezo salama baada ya kutoa hayo maji na wakati wakufanyia usafi bwawa lako.

   ⧫Kwa samaki huyo uliyemtenga unaweza ukawa unaendelea kumtibia taratibu akiwa katika sehemu tengefu isiyochangamana na wenzake.

 ⧫Kwa njia nafuu na za kienyeji kama wewe ni mkulima mdogo unaweza tumia maji ya chumvi kama ni magonjwa ya ngozi kwa kumdumbukiza kwa dakika chache kila siku mpaka utakaapoona amepona vizuri.

 ⧫Usimchanganye na samaki wengine mara tu baada ya kupona,muache kwa muda hata mwezi mzima kwakuwa magonjwa kama fungus yanatabia yakuingia mpaka ndani kwenye damu hivyo yaweza kukudanganya kwa nje kuwa amepona kumbe ndani bado anaugonjwa na kukusababishia hasara ya samakiwako wote.


AHSANTE KWA KUTUMIA MUDA WAKO KUPITIA KAZI ZETU,NA IMANI UTAKUWA UMEJIFUNZA MENGI,USIKOSE KUFUATILIA WAKATI UJAO TUTAJIFUNZA KITU KIPYA KIDOGO KIZURI SANA “UFUGAJI SAMAKI MSETO” HII UNACHANGANYA NA KILIMO CHA KISASA PAMOJA NA UFUGAJI KUKU AMA BATA NA KUKUPA MATOKEO CHANYA BILA KUHARIBU MAZINGIRA KABISA(TUTAJIFUNZA PIA UTENGENEZAJI WA MABWAWA YASIYOHARIBU MAZINGIRA YETU,FUGA SAMAKI BILA KUCHIMBA ARDHI).
LENGO LETU NI KUKUFANYA WEWE KUZIONA FURSA NA KUZITUMIA BILA KUHARIBU MAZINGIRA HUKU UKIKUZA KIPATO CHAKO
AHSANTE SANA NA MUNGU AKUBARIKI!!!