Thursday, 1 March 2018

UFUGAJI SAMAKI MSETO

MKOMBOZI KWA WAFUGAJI WENYE KIPATO KIDOGO!!


Hii ni moja kati ya aina za ufugaji wa samaki wa kutumia gharama nafuu na kuleta faida kubwa kwa wafugaji. 
Aina hii ya ufugaji samaki huenda sambamba na shughuli nyinginezo za kilimo, ufugaji kuku,bata ama nguruwe katika eneo moja ama katika maeneo yaliyokaribiana sana..



 Aina hii ya ufugaji ni ufugaji pekee ulio katika mfumo maalumu wa mlishano wa kutegemeana kati ya samaki unao wafuga,nguruwe,kuku,bata na kilimo utachofanya.Hivyo humpunguzia gharama nyingi sana mfugaji kwani hatakuwa na uhitaji wa kununua mbolea nje kwaajili ya kurutubisha bwawa wakati wa uaandaaji wa bwawa kabla ya kupandikiza vifaranga,mbolea itakayopatikana toka kwa kuku,nguruwe ama bata itatumika kurutubisha maji kwenye bwawa kwaajili ya uzalishaji wa mimea ya majini  (phytoplankton)ambayo ni muhimu sana katika ukuaji wa samaki,lakini vilevile mbolea nyingine itatumika moja kwa moja kwenye mazao kwenye shamba la miti,matunda na vilevile katika bustani ya mbogamboga.

Mbali na hapo katika aina hii ya ufugaji maji machafu yanayo tolewa wakati wa kubadilisha maji toka kwenye bwawa hapa huwa hayamwagwi ovyo,yanaongozwa na mabomba ya kutolea maji ama mifereji toka kwenye bwawa na kuelekezwa kwenye bustani ya mbogamboga na maeneo mengine yenye mazao kama miti ya matunda na mbao iliyozunguuka katika eneo la shamba lako (Maji haya yana mbolea na virutubisho vingi sana hivyo husababisha mimea kubadilika kwa haraka kuwa kijani Zaidi na  kukuwa kwa haraka).

 Vile vile matope,majani,wadudu na takataka nyinginezo zinazotoka ndani ya bwawa wakati wa kubadili maji hutumika kama chakula kwa nguruwe na kuku badala ya kutupwa.
Hivyo unaweza ukajionea aina hii ya ufugaji ilivyo nzuri katika swala la kubana matumizi kwa kuhakikisha kila rasilimali iliyopo inatumika vizuri kwa manufaa ya mfugaji na viumbe husika vinavyofugwa,kuhakikisha eneo lote la shamba lako na rasilimali zote zinatumika kwa manufaa pasipo kutumia gharama kubwa za uwendeshaji mradi.

Aina hii ya ufugaji ni mkombozi hasa kwa wafugaji wenye kipato ama mtaji mdogo,pia aina hii ya ufugaji ni rafiki na mazingira yetu kwa kiasi kikubwa haisababishi uharibifu wa mazingira ukilinga nisha na aina nyinginezo nyingi(sehemu kubwa inajiendesha yenyewe kwa kutumia vitu asili vilivyoko katika mazingira ya kawaida mashambani).

 Aina hiii ya ufugaji mseto pia humpa nafasi kubwa mfugaji ya kuweza kupata faida kubwa Zaidi na kupanua mradi wake kwani anakuwa anafanya shughuli Zaidi ya moja zinazo tegemeana kwa wakati moja na kumletea mavuno endelevu ya bidhaa tofauti kwa vipindi tofauti(mavuno tofauti yasiyokuwa ya msimu na kwa mazao tofauti). 

Mfano:
Mfugaji anapokuwa amefuga samaki aina ya sato ama kambale kwa wingi sambamba na ufugaji kuku wa kiasi,pamoja na kilimo cha mbogamboga kwa eneo dogo lililozunguuka mabwawa yake,eneo kubwa la shamba lililobaki akapanda miti ya matunda na mbao kama tiki(hakika baada ya miezi sita ataanza kuvuna samaki,mbogamboga na matunda na kama akiwa walizingatia upandikizaji wa vifaranga kwenye mabwawa kwa muda tofauti hii itampa uvunaji endelevu wa samaki kwenye ma bwawa yote kila baa da ya miezi sita),Kikubwa Zaidi ni kwamba wakati huwo miti ya mbao na matunda itakuwa ikiendelea kukuwa(miti kama tiki  kwa muda wa miaka kuanzia kumi unakuwa na uhakika wa hela ya kutosha),Miti hii itakusaidia kama mtaji mkubwa utakao kuza mradi wako wakati ujao ili uweze kufuga kisasa Zaidi na kuwa na teknolojia ya kisasa ya ufugaji samaki kwa faida kubwa(kwa mfumo huu unampa fursa mfugaji mwenye kipato kidogo kuwa na uhakika wa kutimiza malengo yake)


             Mpangilio mzuri wa ufugaji samaki mseto kwa mradi mkubwa:




Kwa mawasiliano/mualiko wa kuendesha semina n.k tupigie ama tuandikie kupitia:

+255(0)764175381, +255(0)713199655